Friday, 20 October 2017

TUANGAZIE TAMADUNI ZETU, 'Akakwiliya' MILA ZA MIRATHI KWA WAFIPA, UNDANI WAKE

 
Michezo ya Ngoma na nyimbo za asili, ni jambo la kujivunia kwa kila Mfipa, na ningumu kukuta sherehe zao zozote hakuna michezo au maonyesho ya utamaduni wao, ambapo hutumia vyombo ya kitamaduni, pamoja na vinywaji na vyakula vya kitamaduni.

Mila na desturi za makabila mbalimbali hupaswa kuenziwa na kuendelezwa na jamii husika, (haswa tamaduni nzuri na kutokomeza zile mbaya) ambapo kwa pamoja leo naomba tuangazie kuhusu utamaduni wa Wafipa Urithi wa Mali, Mke baada ya msiba.

UTARATIBU WA KUMALIZA MISIBA NA URITHI
Katika kumaliza kilio kwa Wafipa, jambo la kwanza ambalo mpaka sasa linafanyika ni kuitishwa kwa mkutano wa awali wa ndugu ukiongozwa na Mzee wa boma au wakuu wa ukoo wa kila upande mume na mke, ambapo kwa pamoja hujadili nani atamrithi marehemu (kwa lugha ya kifipa ikijulikana kama ‘akakwiliya’.)
 
KUHUSU URITHI
Wanaoweza kurithiana ni watoto wa baba mkubwa na mdogo, watoto wa mama mkubwa na mdogo, Binamu na pia mtoto anaweza kumrithi baba yake kama ndugu za huyo baba wameisha (hata hivyo urithi huo ni wa kusaidia kumtunza mjane au mgane na sio kuchukua uhusika wa kuwa mke na mume).
 
Pia mjukuu anaweza kumrithi babu au bibi kuwa mume wake au mke wake (kama cheo cha kupewa tu), Mtu na kitukuu wanarithiana kwa hali na mali yaani wanaweza kuchukuliana mke na mume, mtu anaweza kumrithi mjomba wake na mke wa mjomba akawa mke wake nk.
 
Lakini cha kushangaza zaidi katika mila hii ya kurithiana: Msichana anaweza kumrithi shangazi yake na mume wa shangazi akawa mume wake, ambapo Zamani ilikuwa hata shangazi akiwa hai, mathalani akiumwa kwa muda mrefu msichana (Mpwa) wa shangazi alipelekwa kwa shangazi yake ili kumsaidia katika kazi zote hata kulala na baba (Mume wa shangazi) ili kumzuia mumewe huyo asilale nje ya ndoa. Pagumu hapo! Nikulala tu sijui kama kuna mengine yanaendelea……
 
Zamani mrithi hukabidhiwa mali zote za marehemu (haswa mume) ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake wote aliokuwa nao na wao kumpa heshima yake kama baba mpya.
 
Mkutano huu wa ‘Akakwiiya’ kwanza hufanyika kwa siri kidogo ili wanandugu wawe huru kujadili nani haswa anastahili kukabidhiwa jukumu hilo la urithi, ambapo baada ya mkutano huo wa kificho hatimaye hufuatiwa na mkutano wa hadharani ambao kila mtu anayetaka anaweza kuhudhuria.
 
Na mkutano huo unaoongozwa na mkuu wa ukoo kwa upande wa kiumeni, naye huuliza kama kilio au maombolezo yameisha.! Kama watasema yaendelee, basi anaruhusiwa kuuendeleza kwa gharama zake, na kama utakuwa umefika mwisho, basi mjadala wa urithi unafanyika kwa kutoa mapendekezo na maafikiano yaliyopatikana katika kikao cha uficho.
 
Kwa Wafipa wa Milansi kama mtoto wa kwanza katika familia ndiye aliyefariki basi urithi huenda upande wa baba na anapokufa mtoto mwingine inakuwa zamu ya upande wa mama wa marehemu.
 
Baada ya uamuzi kufikiwa wa nani atakuwa mrithi, basi akina mama walioko kwenye chumba cha maombolezo hupelekewa taarifa na wakiafiki huitikia kwa kusema ‘Mwandila ta” na kama hawakubaliani nao hupewa fursa ya kutoa mawazo yao.
 
Endapo akina mama wamekubaliana na uteuzi wa mrithi, basi mama mmoja huchaguliwa kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala, ambapo kama mrithi ametoka upande wa kiumeni basi mfagiaji huwa wa upande wa kikeni na lazima pafagiliwe siku hiyo hiyo.
 
Kwa wafipa vumbi linalotolewa baada ya kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala linamwagwa chooni, Hii ni kwa ajili ya tahadhari ya mchawi kuchukua vumbi hiyo na kufanyia uchawi kama inavyoaminika.
 
Kadhalika, mtu haruhusiwi kuchukua mifupa ya nyama ya kilioni na hii ni kwa tahadhari ya mtu kufanyia uchawi kama Wafipa wanavyoamini.
 
Baadaye watu wote hutangaziwa mrithi ni nani na hapo hutolewa chakula na baada ya chakula watu huondoka.
Kayeemba hupewa nafasi ya kumnawisha mrithi miguu, mikono na uso kwa maji ya uvuguvugu na kisha humpaka mafuta; ikiwemo Vifaa vyote ambavyo vimerithishwa navyo pia hupakwa mafuta.
Maandalizi ya Pombe ya kienyeji kwa kutwanga kwenye kiuri kwa wafipa, katika Maonyesho ya shuhuli zifanywazo na wakinamama wa utamaduni huo , ikihusisha wacheza ngoma za  asili, na maonyesho mengine kuhusu mila na desturi zao hususani wakati wa sherehe.
 
 
Baada ya kupewa vifaa vya urithi husindikizwa kutoka nje ya nyumba na kutembea hatua chache nje ya nyumba na baadaye kurudi. (Hii inakuwa ni kukumbusha vitendo vya marehemu kuwa alikuwa anatoka na kurudi.)
 
Tendo hilo likishafanyika, hutolewa nje viti viwili vinavyokaliwa na mrithi na mrithiwa na hii inakuwa fursa ya kupewa mawaidha kwa lugha ya Wafipa huita ‘Ukusuunda’  na baada ya mawaidha hayo kutolewa hufuatiwa na kitendo cha kunyolewa nywele wahusika.
 
Kwa Wafipa kuonesha huzuni ya kufiwa, wote hupaswa kunyoa nywele zote kichwani (kipara) na hili hufanyika kwa ndugu wote wa marehemu, ambapo Kwa kawaida mrithi na mrithiwa hupaswa kunyoana wenyewe, kisha baada ya kumaliza msiba ilikuwa ni shurti kuenda kuoga maji ya mtoni.
 
Wakati wa maombolezo, waombolezaji hawakuoga; Hivyo baada ya kunyolewa nywele huenda kuoga au kunawa, ikiwa ni njia ya kujitakasa na pepo wabaya ambao wanaweza kuleta kifo.
Pombe ya asili ya kabila la Wafipa inayotengenezwa kwa ulezi na kunyewa kwa kwa kutumia mirija.
Baada ya hapo kinatolewa chakula cha jioni. ‘i chiloosha’.  Mkuu wa ukoo wa upande wa baba alikula kuku na kwa heshima sana alipewa filigisi ‘i’inkushu’ ambayo kwa Wafipa ni nyama ya heshima sana (hailiwi na wote). Naye humega na kugawa kidogo kidogo kwa baadhi ya wanaukoo.
 
Mjumbe au mkuu wa kijiji naye alichinjiwa kuku, ikiwa ina maana kuku wa kusafisha mji, na huyo kuku aliliwa na jumbe pamoja na wazee wengine wa kijiji ili kukisafisha hicho kijiji. Hii kwa wale wapenda kuku, siku kama hizo hawazikosi….
 
Moto wa kilioni pia huzimishwa siku hiyo na mzimishaji huwa ni kayeemba, na Majivu yote hutupwa chooni pia. Kuzimwa kwa moto huo huonesha kwamba kilio kimeisha.
 
HIYO NI KUHUSIANA NA UTAMADUNI WA WAFIPA KATIKA KUMALIZA MISIBA, NA UTAMADUNI WA KURITHISHANA MALI NA WATU – uonavyo wewe ipi hasara na faida ya tamaduni hii….?
 
SOURCE: January Mbalamwezi (mwandishi wa kitabu cha ‘Utamaduni wa Wafipa)
- Wakuu wa Sumbawanga
- Habari Leo (Makala 18792)
- The white Fathers na Ufipa.
- Channel 10.
 
 
TOLEO LIJALO: TUTAANGAZIA KUHUSU ASILI YA NENO SUMBAWANGA NA MWANZILISHI WAKE!
 
Share Pia kama umeipenda na wenzako pia waone na kujifunza.

HARUFU MBAYA YA KINYWA ISIKUFANYE UKOSE KUJIAMINI MBELE YA WENZAKO

Namna sahihi na njia bora ya kusafisha meno, hushauriwa kuwa usiku kabla ya kulala na asubuhi kabla ya kupata kifungua kunywa.

Afya ya kinywa ina umuhimu mkubwa zaidi ya unavyoweza kufikiria kwani huweza kumuweka muhusika katika hali ya kujiamini au kutokujiamini mbele ya wenzake.
 
Ambapo mara nyingi, mtu anaposumbuliwa na kutoa harufu mbaya kinywani, huweza kutengwa waziwazi na wenzake wakiwa katika makundi wakiongea kutokana na harufu mbaya itokayo kinywni na ambayo huwa sio rahisi kuvumilika.

TAMBUA TATIZO:

Kwa ujumla tatizo hili hutokana na muhusika kutokujiwekea utaratibu mzuri wa kusafisha kinywa chake kwa muda mrefu, kutumia mswaki mmoja muda mrefu, pamoja na kuswaki pasipo kuchokonoa mabaki ya vyakula yagandayo kwenye fizi za meno kwa kutumia nyuzi zinazoshauriwa na wataalamuau kutumia vijiti vya meno (tooth-stick) baada ya kula.
 
Mara nyingine muhusika kutokuwaona wataalamu ili kupima na kujua namna ipasayo kuweza kutunza meno yake, au kupewa ufahamu kuhusiana na jinsi afya yako ya mwili ilivyo.
 
Kuelezewa uhusiano uliopo kati ya afya ya kinywa na afya ya mwili mzima kunasaidia kufahamu umuhimu wa kutunza kinywa na hasa meno yako na fizi.
 
Kama zilizo sehemu nyingine za mwili, kinywa nacho kimejaa bakteria ambao wengi wao hawana madhara katika mwili wa binadamu, ambapo Kwa kawaida mfumo wa kulinda mwili na utunzaji mzuri wa kinywa kama vile kupiga mswaki na kutumia uzi kuondoa uchafu katika meno kunaweza kudhibiti bakteria walioko kinywani wabakie katika hali ya kawaida na kutodhuru kinywa chako.
 
Lakini bila kutunza vyema kinywa chako, bakteria hao huweza kusababisha maambukizo kutoka jino moja hadi jino jingine na kusababisha meno yako kuoza na hatimaye kupata maradhi ya fizi, au kung’oa meno yote na kubakia kibogoyo (kutokuwa na meno).
 
NAMNA SAHIHI YA UTUNZAJI WA KINYWA CHAKO
Afya ya kinywa inajumuisha siha na namna ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo hasa meno na fizi, pamoja na namna iliyobora ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo wako zinazofikika na zisizofikika hasa meno na fizi.
 
Mbali na kinywa kutuwezesha ipasavyo kula, kuzungumza na hata kuwa na muonekano mzuri wa uso (kutabasamu na kucheka mbele ya wengine), meno na fizi zinapaswa zisiwe zimedhurika na kuwa na matatizo kama vile meno kuoza, magonjwa ya fizi, kung'oka meno na mdomo kunuka.
 
Kuoza meno na meno kuwa na matundu ni matatizo ya kinywa yanayoshuhudiwa sana miongoni mwa watu wengi kwa miaka ya sasa hasa vijana, ambapo katika rika la miaka 20 – 38 tayari muhusika anakuwa ameng’oa meno mpaka matatu.
 
Sababu zinazoweza kuzuia matatizo hayo ya meno ni kudumisha usafi wa kinywa mara kwa mara, kupata fluoride ya kutosha na kutokula kwa wingi vyakula vinavyoweza kudhuru meno na kusababisha matundu hayo.
 
UHUSIANO AFYA YA KINYWA NA MENO
Afya ya meno na kinywa kwa ujumla inahusiana na afya ya mwili mzima kwa njia tofauti, na aina ya vyakula unavyopendelea kula; sababu kuwa na uwezo wa kutafuna chakula na kukimeza ni muhimu ili mwili wako uweze kupata virutubisho muhimu vya kujenga mwili.
 
Halikadhalika kuwa na kinywa chenye matatizo huweza kuathiri namna mtu anavyozungumza na hata kujiamini kwake mbele za watu walio karibu, kupunguza ufanisi kwa wanandoa, pia matatizo hayo ya meno yanaweza kupelekea gharama kubwa ya matibabu na ukarabati wa meno yako.
 
SABABU ZINAZOPELEKEA KUATHIRI AFYA YA KINYWA NA KUTOA HARUFU MBAYA MDOMONI
Mfano wa mpangilio wa meno, na namna ya fizi zinavyoweza kudhuru meno mdomoni, meno kuwa imara au meno kutotoba.


 

Uimara wa meno na fizi hutofautiana sana kati ya mtu na mtu, na umbo la taya zake, muundo wa mdomo na mpangilio wa meno yake, na hata kiasi cha uchache au wingi wa mate mdomoni mwako.
 

Baadhi ya watu ambao hupendelea kula mara kwa mara vyakula venye sukari nyingi na vyenye siagi, imeeleza na wataalamu kuwa watu hao kwa asilimia kubwa ndio wamekuwa wakisumbuliwa zaidi na matatizo haya, kwani huzalisha kemikali nyingi mdomoni ambazo huruhusu wingi wa asidi au tindikali ambayo nayo humpelekea muhusika kujawa na mate mengi mdomoni.
 
Ambapo kujawa mate huko mdomoni hupelekea kukosa kujiamini kwa muhusika mbele ya wenzao, iwe wakati wa kuongea  au kucheka kwani wamekuwa wakirusha chembe-chembe za mate ambazo huwatoka vinywani mwao pasipo wao wenyewe kujitambua au kuweza kujizuia, na ikifikia wakati huo watu hawa ndio hutengwa waziwazi na wenzao.
 
Kwa uchache, Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yanayoweza kuainishwa kwa nini baadhi ya watu meno yao yanaoza zaidi kuliko wengine, kutoa hurufu mbaya kinywani na kukosa kujiamini au pia baadhi ya watu kuwa na meno dhaifu na wengine kuwa na meno yaliyo imara.
 
SABABU ZA KUTOBOKA KWA MENO
Baadhi ya meno yanaweza kutoboka kwa kuwa na vishimo na nyufa ambazo huweza kuruhusu bakteria na tindikali kupenya kwa urahisi, kutokana na kutafuta sehemu salama ya kujihifadhi ili wasishambuliwe na tindikali hiyo.
 
Ambapo kutokana na nyufa zilizoko katikati ya meno huruhusu mabaki mengi ya vyakula kutwama kwa muda mrefu, na kutoa ulinzi kwa baikteria shambulizi wa meno kutoshambuliwa na tindikali-mate, kwani wakati muhusika akiswaki au kusafisha kinywa chake hushindwa kuzisafisha sehemu hizo zenye mabaki ya vyakula.
 
Na hiyo huchagizwa na maumbo ya baadhi ya taya za watu hao, ambapo taya zao na mpangilio wa meno yao huweza kuzuia meno yasisafishike vizuri na kuondoa vyema uchafu kinywani ulioko katikati ya meno yao “hapa fahamu mpangilio wa meno yako na namna sahihi ya usafishaji wake”.
 
Kiwango cha mabaki ya vyakula vingi haswa vyenye sukari, na uchache wa mate yalivyo mdomoni pia huweza kuathiri uozaji wa meno yako na kutobolewa au kushambuliwa kwa urahisi na wadudu wavamizi.
 
Kwa mfano matundu na nyufa za meno huwa haziko sana katika meno ya mbele ambako kuna mate mengi, ikilinganishwa na meno ya nyuma.
 
Ndio maana meno mengi yanayoanza kushambuliwa na wadudu huwa ni meno ya nyuma (magego) kuliko meno yaliyoko upande wa mbele.
 
KUNUKA KWA MDOMO NA NAMNA SAHIHI YA KUZUIA HARUFU MBAYA YA KINYWA
 
Kutoa harufu mbaya kinywani, huchagizwa na kutokupiga mswaki mara kwa mara, kutumia mswaki mmoja muda mrefu, kutojiwekea utaratibu wa kusafisha mabaki ya chakula yaliyotwama katikati ya meno yako au kwenye fizi.
 
Kupiga mswaki au kusafisha kinywa chako, unashauriwa na wataalamu wa meno kufanya hivyo walau mara mbili kwa siku; ikimaanisha usiku kabla ya kulala na asubuhi kabla ya kupata kifungua kinywa.
 
Watu wengi hapa mmekuwa mkikosea namna bora ya kusafisha kinywa chako, kwa kupiga mswaki na kisha kula ‘hiyo ni makosa’.
 
Wataalamu wanakwambia muda ambao wadudu wanaoshambulia meno (baikteria) ni majira ambayo unakuwa mwili umejipumzisha, na mdomo wako haufanyi kazi “kula au kuongea” hivyo wakati gani muhimu zaidi kwako kupiga mswaki? Jibu unalo!
 
Kuzuia harufu mbaya ya kinywa chako; hakikisha unaswaki mara baada ya kula na kabla ya kulala, ikimaanisha ukishamaliza kula pumzika dakika25 au 30, kisha piga mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye fluoride na madini ya ‘calcium’ kwa wingi.
 
Asubuhi ukishapiga mswaki na kupata kifungua kinywa hakikisha unasukutua maji mdomoni mwako kuondoa mabaki ya chakula au vitafunwa kwenye meno yako.
 
Mwisho kabisa, waone wataalamu kuchunguza afya ya kinywa chako mara kwa mara, kupata ushauri wa namna ya kutunza meno yako yasishambuliwe na wadudu, pamoja na kujiwekea utaratibu wa kusafisha fizi zako kwa kutumia uzi angalau mara3 kwa wiki.
 
Stewart Meena:

Saturday, 14 October 2017

VIUMBE MBALIMBALI HUWEZA KUTOA TAFASIRI HALISI YA MAISHA YA BINADAMU.

Meli ya china iliyofanikisha utafiti huo kwa mara ya kwanza katika Babari ya pasifiki.
 Meli ya utafiti wa sayansi ya China tarehe 14 imefanya uchunguzi kuhusu mlima Caroline ulioko chini ya eneo la magharibi la bahari ya Pasifiki ambao binadamu hawajawahi kuuchunguza, na imekusanya sampuli nyingi za viumbe na jiografia, ikiwemo mnyama aina ya sponji wa rangi ya njano ambaye ni nadra kugunduliwa na sponji aina ya Venus's flower basket ambaye alisifiwa kuwa alama ya "upendo wa kudumu".  Sponji ni myama wa asili zaidi mwenye seli nyingi, hana mdomo na tumbo, huwa na umbo linalofanana na chupa, nguzo au kikombe, na ana mashimo mengi mwilini, hivyo viumbe wengi wanapenda kuishi ndani ya sponji.

Sampuli ya sponji wa rangi ya njano ina urefu wa sentimita 80. Watafiti wamesema sponji mkubwa wa rangi hii ni nadra kuona, na sponji wa kawaida huwa ni mweupe.

Watafiti pia wamegundua sponji aina ya Venus's flower basket. (Pichani chini) Kamba aina ya Spongicola jike na dume wanapokuwa wadogo, huingia mwilini mwa sponji kupitia kwenye tundu zake. Kuishi ndani ya sponji ni salama, na bado wanaweza kupata chakula. Baadaye kamba hao wanakua na kuwa wakubwa, hawawezi kutoka tena. Dume na jike wanaishi huko maishani yao yote. Hivyo watu wa baadhi ya nchi wanawachukulia sponji wa aina hiyo kama alama ya "upendo wa kudumu.


source: China Radio blog.

ZINGATIA MUDA SAHIHI WA MAPUMZIKO KUBORESHA AFYA YAKO

AFYA YAKO:
Imeebainika kuwa katika nchi nyingi za kiafrika, Tanzania ikiwemo watu wengi huchelewa kulala (Haswa vijana) kwa kutumia muda wao wa Usiku baada ya kazi za kutwa kutizama Filamu. Na stewart meena
 
Je wajua, Ukosefu wa usingizi huwafanya watu kujisikia uwezo wao umepungua katika utendaji wa mambo mbalimbali katika maisha yao ya kila siku? Utafiti mpya uliotolewa na Chuo kikuu cha Leeds umeonesha kuwa ukosefu wa usingizi unaweza kuathiri afya ya kiakili na uwezo wa kumbukumbu.  Watafiti wa Chuo hicho walishirikiana na kampuni moja kufanya utafiti mkubwa uliowashirikisha watu zaidi ya elfu moja wa Uingereza wenye umri kutoka miaka 18 hadi 80. Watafiti waliwataka watu hao kujaza fomu kuhusu tabia za kulala, uwezo wa kumbukumbu, hali ya kisaikolojia na hali ya maisha, na kutafiti matokeo ya takwimu hizo. Watafiti wamesema, kutokana na takwimu, ukosefu wa usingizi una uhusiano mkubwa na kushuka kwa afya ya kiakili na kuwa mbaya kwa uwezo wa kumbukumbu, haswa kwa wale wanaolala kwa muda usiozidi saa tano, uhusiano huo utakuwa mkubwa zaidi. Kwa mfano wanaweza kusahau jukumu wanalotakiwa kufanya, kusahau mahali ambako jambo lilitokea au kusahau jambo walilopanga. Hivi sasa mfumo wa afya ya umma wa Uingereza umependekeza watu wazima kulala saa 7 hadi 8 kila usiku. je wewe huwa unalala masaa mangapi?

Tuesday, 29 August 2017

KOREA NA MIPANGO YAKE HASI HATUA NYINGINE ZAIDI.

HEBU TUJIFUNZE KITU LEO KUHUSIANA NA KOREA KASKAZINI NA CHOKOCHOKO DHIDI YAKE NA MAREKANI:
Source: BBC SWAHILI http://www.bbc.com/swahili/habari-41084338

Ni kwa nini Korea Kaskazini inataka silaha za nyuklia?