Na. Stewart Meena.
Moshi ni wilaya na makao makuu ya Mkoa wa
Kilimanjaro, mkoa mmojawapo ambao unaunda nchi ya Tanzania, Na ikiwa imegawanyika
katika kanda mbili ile ya (Moshi mjini) na ile ya (Moshi Vijijini).
Mkoa wa Kilimanjaro umegawanyika katika wilaya
7 ambazo ni: Hai, Siha, Moshi mjini, Moshi vijijini, Rombo, Mwanga na Same.
LEO Tunaiangazia Wilaya hii ya MOSHI: Ambayo
kimsingi ni miongoni mwa wilaya kongwe Tanzania kiasi kwamba baadhi ya watu
kwingineko ‘Mikoani’ wamekua wakiihusisha Wilaya hii na Mkoa na kusahau kuwa
mkoa ni Kilimanjaro na sio Moshi kama wadhaniavyo.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka
2022, Mkoa wa Kilimanjaro una idadi ya wakazi wapatao "Milioni1 Laki8 na
elfu61, mia9 na34, Huku Wilaya ya Moshi Mjini na ile ya moshi vijijini pekee,
ina jumla ya wakaazi wapatao Laki8, elfu67, mia5 na 36 (331,733 - Moshi mjini,
na 535,803-Moshi vijijini) ingawa hii huweza kupanda maradufu haswa wakati wa
sikukuu ya krismass na mwaka mpya, wenyeji wanapokuwa wamerejea kutoka mikoani kwenye
utafutaji (wenyewe wakiita "kurudi kuhesabiwa")
Kabila linaloongoza kwa idadi kubwa ya wakazi
wa mji wa Moshi ni: Wachaga wakifuatiwa na Wapare, Wagweno wa wilaya ya Same na
Mwanga, na makabila mengine madogo-madogo yaliyohamia kutoka sehemu mbalimbali
za Tanzania kama Wadigo na Wasambaa (wagosi) kutoka mkoa wa Tanga, Waarusha,
waMeru na Wamasai kutoka Mkoa wa Arusha, Warangi-Kondoa, waPemba-Zanzibar, n.k.
huku kukiwa na wale wageni kutoka nchi jirani ya kenya: Wakuitwa WaKamba,
Wajaluo, waKahe na waTaita, kutokea eneo la Taveta, Mombasa-Kenya.
Zifuatazo ni kata za Wilaya ya Moshi (Mjini na
Vijijini)
Moshi mjini:
KATA ZA MOSHI MJINI: Bomambuzi, Bondeni,
Kaloleni, Karanga, Kiboroloni, Kilimanjaro, Kiusa, Korongoni, Longuo A na B,
Majengo, Mawenzi, Mfumuni, Miembeni, Mji Mpya, Msaranga, Ng'ambo, Njoro, Pasua,
Rau (juu), Shirimatunda na Soweto.
Arusha Chini, Kahe Magharibi, Kahe Mashariki,
Kibosho, Kibosho Kati, Kibosho Kirima, Kibosho Magharibi, Kibosho Mashariki,
Kilanya, Kilema Kaskazini, Kilema Kati, Kilema Kusini na Maporomoko ya maji
Materuni.
NYINGINE: Okaoni, Old Moshi Magharibi, Old
Moshi Mashariki, Sambarai, Uru Kaskazini, Uru Kusini, Uru Mashariki, na Uru,
Shimbwe.
Moshi Vijijini
KATA ZA MOSHI VIJIJINI: Mamba Kaskazini, Mamba
Kusini, Manushi, Marangu, Marangu Magharibi, Marangu Mashariki, Mbokomu, Mwika
Kaskazini, Mwika Kusini, Njia Panda (Himo), Nyumba ya Mungu, Kimochi, Kindi,
Kirua Vunjo Kusini, Kirua Vunjo Magharibi, Kirua Vunjo Mashariki, Lyamungo,
Mabogini, Kahe, na Makuyuni (Himo).
VYAKULA:
Vyakula vya asili haswa kwa Wachagga
hupendelea zaidi vyakula vinavyopikwa kwa kutumia Nafaka, ndizi, magimbi (mayugwa),
maziwa na nyama. Mfano: Mtori (Hupikwa kwa ndizi zilizosagwa na nyama), kitawa
(Ndizi na maziwa mtindi), kyumbo (Ndizi na maharagwe), na machalari, (Ndizi na
nyama) pamoja na Ng'ande.
Nafaka zilimwazo ni pamoja na" kunde,
maharage, ulezi, mtama, alizeti na mahindi" Huku mifugo kama mbuzi,
ngombe, nguruwe na kondoo, na ile ya jamii za ndege kama bata, kuku, na kanga
wakifugwa pia kwa wingi kwaajili ya biashara, nyama mayai na maziwa kwa mbuzi
na ng’ombe.
Kwa utajiri huo wa mazao ya nafaka: Moshi
hupelekea kutengenezwa na kutumiwa kwa vinywaji vyenye kilevi na visivyo na
kilevi (pombe) mbalimbali, na ni vya asili maeneo haya, ziitwazo, Dadii (mchanganyo
wa unga wa mahindi), togwa (kutumia mtama), na "Mbekee au mbege,
inayopikwa kwa kuchanganya (ndizi, ulezi na mti wa msesewe) ambacho ndio
kinywaji pendwa zaidi wilayani hapa.
Wakazi wengi wa Moshi ni wakulima, wafugaji na
wafanyabiashara, ambapo eneo kuu la biashara ni masokoni, na masoko makuu eneo
hilo ni: Mwika, Kisambo, Kiraracha, Kiusa, Marangu mtoni, Himo, Kiboroloni,
Mbuyuni, Kahe (Chekereni) na Soko kuu la mitumba Memorial njia ya kuelekea Mkoa
jirani wa Arusha.
Katikati ya mwaka, idadi ya wakazi wa maeneo
haya hupungua, haswa vijijini maana watu wake wametawanyika miji mbalimbali
Tanzania, kwaajili ya kufanya biashara na utafutaji, huku wale waishio
vijijini, huenda marangu mtoni, Mwika, moshi mjini, au Himo kufanya kazi na kurudi
nyumbani jioni giza linapozama.
Na hii ndio maana utasikia watu wakisema: “Utakapoenda
popote Tanzania ukamkosa mchaga na msambaa, na Muha basi ondoka hapo hapafai
kuishi”
UKUAJI WA UCHUMI:
Ukuaji wa mji wa Moshi hauendani na mipango
halisi ya 'Mipango Miji'. Hii inatokana na kutokufuatiliwa kwa sheria
mbalimbali zinazohusu uendelezaji wa miji, kutokana na mila za kurithishana
mali na mashamba au viwanja nk. Ikishamiri zaidi maeneo ya vijijini zaidi kuliko
mjini.
HALI YA HEWA:
Moshi ni mji wenye baridi katika miezi ya Juni
mpaka Agosti na joto katika miezi ya Oktoba hadi katikati ya Januari, ingawa
kuna maeneo haswa yanayoelekea mlima Kibo (Kilimanjaro) baridi haikauki majira
yote ya mwaka haswa nyakati za usiku. (Huwezi kulala bila blanketi la
kujifunika) mkoa wote wa Kilimanjaro upo nyanda za juu kaskazini.
SHUGHULI ZA KIUCHUMI:
Kilmanjaro: Uchumi hutegemea zaidi, (Utalii),
kuwapokea wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja kutalii mlima kilimanjaro,
mbuga za wanyama na maporomoko ya maji (Waterfalls) Kuogelea na kujifunza
tamaduni za jadi zaidi zile ziwahusuzo Wamasai waihio Arusha-chini na Kahe.
Maporomoko ya maji mashuhuri zaidi hapa ni
yale ya (Materuni waterfalls), huku kuogelea hupendelea zaidi, marangu, au ile
ya (Kikuletwa) au chemka, iliyopo wilaya ya hai eneo la boma, kujionea samaki
wanaofanya Masaji kufurahia maji joto yake.
Mkoa wa Kilimanjaro na mji wa Moshi una mandhari
nzuri ya kuvutia watalii, na huduma muhimu kama mahoteli, usafiri (ndege na mabasi),
na ukarimu wa wenyeji.
Watalii hupenda sana mji wa Moshi kwa sababu
ya mlima Kilimanjaro, ambao hupandwa kupitia njia tofauti-tofauti zaidi ile ya
kibosho, machame-umbwe, Marangu na Rombo.
Hivyo kusaidia kukuza uchumi wa mji huu wa
Moshi; na kutunza amali na historia ya mji huu, na jirani yake mkoa wa Arusha
wenye mbuga za wanayama mashuhuri za Serengeti, Ngorongoro, Tarangire na Ziwa
Manyara.
MAENDELEO YA ELIMU:
Mji wa Moshi una vyuo vikuu vinne: MUCCoBS
(Moshi University College Of Cooperative and Business Studies) ambacho ni chuo
kikuu kishiriki cha Sokoine University of Agriculture (SUA) ya Morogoro.
MWUCE (Mwenge University College Of Education)
ambacho ni chuo kikuu kishiriki cha SAUT (St. Augustine University - Mwanza); KCMC
Medical School chini ya Chuo Kikuu cha Tumaini; OUT (The Open University of
Tanzania) ambacho ni tawi la chuo chenye jina hilohilo chenye makao yake makuu
jijini Dar es Salaam.
Je! Wajua?
Neno ‘mpare’ ni neno la asili ya kichaga,
likimaanisha (mpige!)
HADI WAKATI UJAO; MAKALA YA MJI WA MOSHI INAISHIA
HAPA….
Tafadhali, (Follow us) Like page na share
ujumbe unaokuvutia kuelimisha wengine pia nao wapate kujifunza kuhusu Tanzania nay
ale yaliyowazunguka.
Facebook #EliaStewartJr. #Special4fans #HistoryAndAmazingThings


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni