Namna sahihi na njia bora ya kusafisha meno, hushauriwa kuwa usiku kabla ya kulala na asubuhi kabla ya kupata kifungua kunywa. |
Afya ya kinywa ina umuhimu mkubwa zaidi ya unavyoweza kufikiria kwani huweza kumuweka muhusika katika hali ya kujiamini au kutokujiamini mbele ya wenzake.
Ambapo mara nyingi,
mtu anaposumbuliwa na kutoa harufu mbaya kinywani, huweza kutengwa waziwazi na
wenzake wakiwa katika makundi wakiongea kutokana na harufu mbaya itokayo
kinywni na ambayo huwa sio rahisi kuvumilika.
TAMBUA TATIZO:
Kwa ujumla tatizo hili
hutokana na muhusika kutokujiwekea utaratibu mzuri wa kusafisha kinywa chake
kwa muda mrefu, kutumia mswaki mmoja muda mrefu, pamoja na kuswaki pasipo
kuchokonoa mabaki ya vyakula yagandayo kwenye fizi za meno kwa kutumia nyuzi zinazoshauriwa
na wataalamuau kutumia vijiti vya meno (tooth-stick) baada ya kula.
Mara nyingine muhusika
kutokuwaona wataalamu ili kupima na kujua namna ipasayo kuweza kutunza meno
yake, au kupewa ufahamu kuhusiana na jinsi afya yako ya mwili ilivyo.
Kuelezewa uhusiano
uliopo kati ya afya ya kinywa na afya ya mwili mzima kunasaidia kufahamu
umuhimu wa kutunza kinywa na hasa meno yako na fizi.
Kama zilizo sehemu
nyingine za mwili, kinywa nacho kimejaa bakteria ambao wengi wao hawana madhara
katika mwili wa binadamu, ambapo Kwa kawaida mfumo wa kulinda mwili na utunzaji
mzuri wa kinywa kama vile kupiga mswaki na kutumia uzi kuondoa uchafu katika
meno kunaweza kudhibiti bakteria walioko kinywani wabakie katika hali ya
kawaida na kutodhuru kinywa chako.
Lakini bila kutunza
vyema kinywa chako, bakteria hao huweza kusababisha maambukizo kutoka jino moja
hadi jino jingine na kusababisha meno yako kuoza na hatimaye kupata maradhi ya
fizi, au kung’oa meno yote na kubakia kibogoyo (kutokuwa na meno).
NAMNA SAHIHI YA
UTUNZAJI WA KINYWA CHAKO
Afya ya kinywa
inajumuisha siha na namna ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo hasa meno na
fizi, pamoja na namna iliyobora ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo wako
zinazofikika na zisizofikika hasa meno na fizi.
Mbali na kinywa
kutuwezesha ipasavyo kula, kuzungumza na hata kuwa na muonekano mzuri wa uso
(kutabasamu na kucheka mbele ya wengine), meno na fizi zinapaswa zisiwe
zimedhurika na kuwa na matatizo kama vile meno kuoza, magonjwa ya fizi,
kung'oka meno na mdomo kunuka.
Kuoza meno na meno
kuwa na matundu ni matatizo ya kinywa yanayoshuhudiwa sana miongoni mwa watu
wengi kwa miaka ya sasa hasa vijana, ambapo katika rika la miaka 20 – 38 tayari
muhusika anakuwa ameng’oa meno mpaka matatu.
Sababu zinazoweza
kuzuia matatizo hayo ya meno ni kudumisha usafi wa kinywa mara kwa mara, kupata
fluoride ya kutosha na kutokula kwa wingi vyakula vinavyoweza kudhuru meno na
kusababisha matundu hayo.
UHUSIANO AFYA YA
KINYWA NA MENO
Afya ya meno na kinywa
kwa ujumla inahusiana na afya ya mwili mzima kwa njia tofauti, na aina ya
vyakula unavyopendelea kula; sababu kuwa na uwezo wa kutafuna chakula na
kukimeza ni muhimu ili mwili wako uweze kupata virutubisho muhimu vya kujenga
mwili.
Halikadhalika kuwa na
kinywa chenye matatizo huweza kuathiri namna mtu anavyozungumza na hata
kujiamini kwake mbele za watu walio karibu, kupunguza ufanisi kwa wanandoa, pia
matatizo hayo ya meno yanaweza kupelekea gharama kubwa ya matibabu na ukarabati
wa meno yako.
SABABU ZINAZOPELEKEA
KUATHIRI AFYA YA KINYWA NA KUTOA HARUFU MBAYA MDOMONI
Mfano wa mpangilio wa meno, na namna ya fizi zinavyoweza kudhuru meno mdomoni, meno kuwa imara au meno kutotoba. |
Uimara wa meno na fizi
hutofautiana sana kati ya mtu na mtu, na umbo la taya zake, muundo wa mdomo na
mpangilio wa meno yake, na hata kiasi cha uchache au wingi wa mate mdomoni
mwako.
Baadhi ya watu ambao hupendelea kula mara kwa mara vyakula venye sukari
nyingi na vyenye siagi, imeeleza na wataalamu kuwa watu hao kwa asilimia kubwa
ndio wamekuwa wakisumbuliwa zaidi na matatizo haya, kwani huzalisha kemikali
nyingi mdomoni ambazo huruhusu wingi wa asidi au tindikali ambayo nayo
humpelekea muhusika kujawa na mate mengi mdomoni.
Ambapo kujawa mate huko mdomoni hupelekea kukosa kujiamini kwa muhusika
mbele ya wenzao, iwe wakati wa kuongea
au kucheka kwani wamekuwa wakirusha chembe-chembe za mate ambazo
huwatoka vinywani mwao pasipo wao wenyewe kujitambua au kuweza kujizuia, na
ikifikia wakati huo watu hawa ndio hutengwa waziwazi na wenzao.
Kwa uchache, Hayo ni
baadhi tu ya mambo muhimu yanayoweza kuainishwa kwa nini baadhi ya watu meno yao
yanaoza zaidi kuliko wengine, kutoa hurufu mbaya kinywani na kukosa kujiamini au
pia baadhi ya watu kuwa na meno dhaifu na wengine kuwa na meno yaliyo imara.
SABABU ZA KUTOBOKA KWA
MENO
Baadhi ya meno
yanaweza kutoboka kwa kuwa na vishimo na nyufa ambazo huweza kuruhusu bakteria
na tindikali kupenya kwa urahisi, kutokana na kutafuta sehemu salama ya
kujihifadhi ili wasishambuliwe na tindikali hiyo.
Ambapo kutokana na nyufa
zilizoko katikati ya meno huruhusu mabaki mengi ya vyakula kutwama kwa muda
mrefu, na kutoa ulinzi kwa baikteria shambulizi wa meno kutoshambuliwa na
tindikali-mate, kwani wakati muhusika akiswaki au kusafisha kinywa chake
hushindwa kuzisafisha sehemu hizo zenye mabaki ya vyakula.
Na hiyo huchagizwa na
maumbo ya baadhi ya taya za watu hao, ambapo taya zao na mpangilio wa meno yao huweza
kuzuia meno yasisafishike vizuri na kuondoa vyema uchafu kinywani ulioko
katikati ya meno yao “hapa fahamu mpangilio wa meno yako na namna sahihi ya
usafishaji wake”.
Kiwango cha mabaki ya
vyakula vingi haswa vyenye sukari, na uchache wa mate yalivyo mdomoni pia
huweza kuathiri uozaji wa meno yako na kutobolewa au kushambuliwa kwa urahisi na
wadudu wavamizi.
Kwa mfano matundu na
nyufa za meno huwa haziko sana katika meno ya mbele ambako kuna mate mengi, ikilinganishwa
na meno ya nyuma.
Ndio maana meno mengi
yanayoanza kushambuliwa na wadudu huwa ni meno ya nyuma (magego) kuliko meno
yaliyoko upande wa mbele.
KUNUKA KWA MDOMO NA
NAMNA SAHIHI YA KUZUIA HARUFU MBAYA YA KINYWA
Kutoa harufu mbaya kinywani, huchagizwa na kutokupiga mswaki mara kwa
mara, kutumia mswaki mmoja muda mrefu, kutojiwekea utaratibu wa kusafisha
mabaki ya chakula yaliyotwama katikati ya meno yako au kwenye fizi.
Kupiga mswaki au kusafisha kinywa chako, unashauriwa na wataalamu wa meno
kufanya hivyo walau mara mbili kwa siku; ikimaanisha usiku kabla ya kulala na
asubuhi kabla ya kupata kifungua kinywa.
Watu wengi hapa mmekuwa mkikosea namna bora ya kusafisha kinywa chako,
kwa kupiga mswaki na kisha kula ‘hiyo ni makosa’.
Wataalamu wanakwambia muda ambao wadudu wanaoshambulia meno (baikteria)
ni majira ambayo unakuwa mwili umejipumzisha, na mdomo wako haufanyi kazi “kula
au kuongea” hivyo wakati gani muhimu zaidi kwako kupiga mswaki? Jibu unalo!
Kuzuia harufu mbaya ya kinywa chako; hakikisha unaswaki mara baada ya
kula na kabla ya kulala, ikimaanisha ukishamaliza kula pumzika dakika25 au 30,
kisha piga mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye fluoride na madini ya
‘calcium’ kwa wingi.
Asubuhi ukishapiga mswaki na kupata kifungua kinywa hakikisha unasukutua
maji mdomoni mwako kuondoa mabaki ya chakula au vitafunwa kwenye meno yako.
Mwisho kabisa, waone wataalamu kuchunguza afya ya kinywa chako mara kwa
mara, kupata ushauri wa namna ya kutunza meno yako yasishambuliwe na wadudu, pamoja
na kujiwekea utaratibu wa kusafisha fizi zako kwa kutumia uzi angalau mara3 kwa
wiki.
Stewart Meena:
E-mail: stewartmeena6@gmail.com
No comments:
Post a Comment