Friday, 20 October 2017

TUANGAZIE TAMADUNI ZETU, 'Akakwiliya' MILA ZA MIRATHI KWA WAFIPA, UNDANI WAKE

 
Michezo ya Ngoma na nyimbo za asili, ni jambo la kujivunia kwa kila Mfipa, na ningumu kukuta sherehe zao zozote hakuna michezo au maonyesho ya utamaduni wao, ambapo hutumia vyombo ya kitamaduni, pamoja na vinywaji na vyakula vya kitamaduni.

Mila na desturi za makabila mbalimbali hupaswa kuenziwa na kuendelezwa na jamii husika, (haswa tamaduni nzuri na kutokomeza zile mbaya) ambapo kwa pamoja leo naomba tuangazie kuhusu utamaduni wa Wafipa Urithi wa Mali, Mke baada ya msiba.

UTARATIBU WA KUMALIZA MISIBA NA URITHI
Katika kumaliza kilio kwa Wafipa, jambo la kwanza ambalo mpaka sasa linafanyika ni kuitishwa kwa mkutano wa awali wa ndugu ukiongozwa na Mzee wa boma au wakuu wa ukoo wa kila upande mume na mke, ambapo kwa pamoja hujadili nani atamrithi marehemu (kwa lugha ya kifipa ikijulikana kama ‘akakwiliya’.)
 
KUHUSU URITHI
Wanaoweza kurithiana ni watoto wa baba mkubwa na mdogo, watoto wa mama mkubwa na mdogo, Binamu na pia mtoto anaweza kumrithi baba yake kama ndugu za huyo baba wameisha (hata hivyo urithi huo ni wa kusaidia kumtunza mjane au mgane na sio kuchukua uhusika wa kuwa mke na mume).
 
Pia mjukuu anaweza kumrithi babu au bibi kuwa mume wake au mke wake (kama cheo cha kupewa tu), Mtu na kitukuu wanarithiana kwa hali na mali yaani wanaweza kuchukuliana mke na mume, mtu anaweza kumrithi mjomba wake na mke wa mjomba akawa mke wake nk.
 
Lakini cha kushangaza zaidi katika mila hii ya kurithiana: Msichana anaweza kumrithi shangazi yake na mume wa shangazi akawa mume wake, ambapo Zamani ilikuwa hata shangazi akiwa hai, mathalani akiumwa kwa muda mrefu msichana (Mpwa) wa shangazi alipelekwa kwa shangazi yake ili kumsaidia katika kazi zote hata kulala na baba (Mume wa shangazi) ili kumzuia mumewe huyo asilale nje ya ndoa. Pagumu hapo! Nikulala tu sijui kama kuna mengine yanaendelea……
 
Zamani mrithi hukabidhiwa mali zote za marehemu (haswa mume) ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake wote aliokuwa nao na wao kumpa heshima yake kama baba mpya.
 
Mkutano huu wa ‘Akakwiiya’ kwanza hufanyika kwa siri kidogo ili wanandugu wawe huru kujadili nani haswa anastahili kukabidhiwa jukumu hilo la urithi, ambapo baada ya mkutano huo wa kificho hatimaye hufuatiwa na mkutano wa hadharani ambao kila mtu anayetaka anaweza kuhudhuria.
 
Na mkutano huo unaoongozwa na mkuu wa ukoo kwa upande wa kiumeni, naye huuliza kama kilio au maombolezo yameisha.! Kama watasema yaendelee, basi anaruhusiwa kuuendeleza kwa gharama zake, na kama utakuwa umefika mwisho, basi mjadala wa urithi unafanyika kwa kutoa mapendekezo na maafikiano yaliyopatikana katika kikao cha uficho.
 
Kwa Wafipa wa Milansi kama mtoto wa kwanza katika familia ndiye aliyefariki basi urithi huenda upande wa baba na anapokufa mtoto mwingine inakuwa zamu ya upande wa mama wa marehemu.
 
Baada ya uamuzi kufikiwa wa nani atakuwa mrithi, basi akina mama walioko kwenye chumba cha maombolezo hupelekewa taarifa na wakiafiki huitikia kwa kusema ‘Mwandila ta” na kama hawakubaliani nao hupewa fursa ya kutoa mawazo yao.
 
Endapo akina mama wamekubaliana na uteuzi wa mrithi, basi mama mmoja huchaguliwa kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala, ambapo kama mrithi ametoka upande wa kiumeni basi mfagiaji huwa wa upande wa kikeni na lazima pafagiliwe siku hiyo hiyo.
 
Kwa wafipa vumbi linalotolewa baada ya kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala linamwagwa chooni, Hii ni kwa ajili ya tahadhari ya mchawi kuchukua vumbi hiyo na kufanyia uchawi kama inavyoaminika.
 
Kadhalika, mtu haruhusiwi kuchukua mifupa ya nyama ya kilioni na hii ni kwa tahadhari ya mtu kufanyia uchawi kama Wafipa wanavyoamini.
 
Baadaye watu wote hutangaziwa mrithi ni nani na hapo hutolewa chakula na baada ya chakula watu huondoka.
Kayeemba hupewa nafasi ya kumnawisha mrithi miguu, mikono na uso kwa maji ya uvuguvugu na kisha humpaka mafuta; ikiwemo Vifaa vyote ambavyo vimerithishwa navyo pia hupakwa mafuta.
Maandalizi ya Pombe ya kienyeji kwa kutwanga kwenye kiuri kwa wafipa, katika Maonyesho ya shuhuli zifanywazo na wakinamama wa utamaduni huo , ikihusisha wacheza ngoma za  asili, na maonyesho mengine kuhusu mila na desturi zao hususani wakati wa sherehe.
 
 
Baada ya kupewa vifaa vya urithi husindikizwa kutoka nje ya nyumba na kutembea hatua chache nje ya nyumba na baadaye kurudi. (Hii inakuwa ni kukumbusha vitendo vya marehemu kuwa alikuwa anatoka na kurudi.)
 
Tendo hilo likishafanyika, hutolewa nje viti viwili vinavyokaliwa na mrithi na mrithiwa na hii inakuwa fursa ya kupewa mawaidha kwa lugha ya Wafipa huita ‘Ukusuunda’  na baada ya mawaidha hayo kutolewa hufuatiwa na kitendo cha kunyolewa nywele wahusika.
 
Kwa Wafipa kuonesha huzuni ya kufiwa, wote hupaswa kunyoa nywele zote kichwani (kipara) na hili hufanyika kwa ndugu wote wa marehemu, ambapo Kwa kawaida mrithi na mrithiwa hupaswa kunyoana wenyewe, kisha baada ya kumaliza msiba ilikuwa ni shurti kuenda kuoga maji ya mtoni.
 
Wakati wa maombolezo, waombolezaji hawakuoga; Hivyo baada ya kunyolewa nywele huenda kuoga au kunawa, ikiwa ni njia ya kujitakasa na pepo wabaya ambao wanaweza kuleta kifo.
Pombe ya asili ya kabila la Wafipa inayotengenezwa kwa ulezi na kunyewa kwa kwa kutumia mirija.
Baada ya hapo kinatolewa chakula cha jioni. ‘i chiloosha’.  Mkuu wa ukoo wa upande wa baba alikula kuku na kwa heshima sana alipewa filigisi ‘i’inkushu’ ambayo kwa Wafipa ni nyama ya heshima sana (hailiwi na wote). Naye humega na kugawa kidogo kidogo kwa baadhi ya wanaukoo.
 
Mjumbe au mkuu wa kijiji naye alichinjiwa kuku, ikiwa ina maana kuku wa kusafisha mji, na huyo kuku aliliwa na jumbe pamoja na wazee wengine wa kijiji ili kukisafisha hicho kijiji. Hii kwa wale wapenda kuku, siku kama hizo hawazikosi….
 
Moto wa kilioni pia huzimishwa siku hiyo na mzimishaji huwa ni kayeemba, na Majivu yote hutupwa chooni pia. Kuzimwa kwa moto huo huonesha kwamba kilio kimeisha.
 
HIYO NI KUHUSIANA NA UTAMADUNI WA WAFIPA KATIKA KUMALIZA MISIBA, NA UTAMADUNI WA KURITHISHANA MALI NA WATU – uonavyo wewe ipi hasara na faida ya tamaduni hii….?
 
SOURCE: January Mbalamwezi (mwandishi wa kitabu cha ‘Utamaduni wa Wafipa)
- Wakuu wa Sumbawanga
- Habari Leo (Makala 18792)
- The white Fathers na Ufipa.
- Channel 10.
 
 
TOLEO LIJALO: TUTAANGAZIA KUHUSU ASILI YA NENO SUMBAWANGA NA MWANZILISHI WAKE!
 
Share Pia kama umeipenda na wenzako pia waone na kujifunza.

No comments:

Post a Comment