Thursday, 17 September 2026

UCHAWI, UHUSIANO - ELIMU KUHUSU VIUMBE WASIOONEKANA!



Elimu kuhusu uchawi na majini ni mada pana inayochukua nafasi kubwa katika imani za kijamii, kitamaduni, na kidini (hususan katika dini kuu zilizopo (Mfano: Ile ya Kiislamu na Kikristo), katika mabara yote saba katika sayari hii ya tatu (Dunia) katika mzunguko wa sayari zote kulizunguka jua.

Afrika na zaidi ikiwemo Afrika Mashariki, Pengine uchawi na elimu kuhusu viumbe wasionekana kwa macho ya kibinadamu (Majini) hutumika tofauti sana na ustaarabu wa maeneo mengine duniani, mfano barani Ulaya, America, na Asia – hutumia elimu hii kwa maswala ya utajiri na mali, teknolojia na maswala ya ki-injinia nk. Tofauti na Afrika hutumika kulogana na kutiana uchizi, kuchuma kwa kuiba mali za wengine (Chuma ulete nk.)

Uchawi kwa bara letu la Afrika, huhusishwa na kuwanga ‘Yaani kuzunguka katika majumba ya watu usiku  na kuwatia zongo nanuksi kwa kuwanenea maneno ya kichawi, na kwa mila na Imani zao yale waliyoyanenea hutukia kwa walengwa waliowakusudia.

MAJINI:

(Mitazamo Ya Kidini Na Kijamii (Ukristo na Uislamu)

By Nancystodd - Icon-religion.svg-Wikipedia


UISLAMU: Kuhusu Majini (Majinn)

Katika mafundisho ya kidini (hasa ile ya Kiislamu), majini ni viumbe halisi walioumbwa na Allah; Ikiwa ni tofauti na binadamu walioumbwa kwa asili ya UDONGO (Adamu na Hawa) na Malaika walioumbwa kwa NURU, Majini waliumbwa kwa MOTO usio na moshi (moto wa upepo mkali).

UKRISTO: Kuhusu Majini (Mapepo/Demons)

'bofya kiungo kwenyemaneno yaliyopigiwa mstari'

Katika mafundisho ya uKristo, yamejikita zaidi kuelezea namna binadamu wa kwanza alivyoumbwa, kisha baadae mwanamke (Adam na Eva), na baadhi ya vitabu kama (Kitabu cha HENOKO ‘Enoch’) Kikiwa kimechambua kuhusu uchawi, majini nk. Kikiondolewa na kutotumika kabisa kwa madhehebu yaliyo mengi ndani ya ukristo, Zaidi kikibakia kutumiwa na Kanisa na ambalo pekee linalokitambua kitabu hicho kama sehemu ya maandiko yao matakatifu ni Kanisa la Kiorthodoksi la Tewahedo la nchini Ethiopia.

Kitabu cha Henoko (kwa Kiingereza: The Book of Enoch) ni mkusanyo wa maandishi ya kale ya kidini ya Kiyahudi yanayonasibishwa na Henoko, babu mkuu wa Nuhu; Ingawa kilitungwa kati ya karne ya 3 na ya 2 K.K, kitabu hiki hakimo katika kanoni rasmi ya Biblia inayotumiwa na Wayahudi na madhehebu mengi ya Kikristo Duniani.



SIFA ZA MAJINI:

Uhuru wa Kuchagua: Imeelezwa kwenye uislamu, kama walivyo wanadamu, majini wana uhuru wa kuchagua kuwa wema (waumini) au wabaya (makafiri); ambapo Jini mbaya au kafiri mara nyingi huitwa Shaytani (Shetani) au Ibilisi.

Maisha Yao: Imeelezwa (Kwenye simulizi za Imam-Shafii) kuwa: wanaishi, wanakula, wanazaa, wanasafiri, na wanakufa kama ilivyo kwa wanadamu, na upekee mkubwa walionao ni kuwa wao wanauwezo wa kutuona wanadamu, lakini wanadamu/binadamu hawezi kuwaona katika umbo lao la asili.

AINA ZA MAJINI NA MAKAZI:

Kwa mujibu wa maandiko mbalimbali, wamegawanyika katika makundi makuu matatu: Wenye mbawa na wanaoruka angani; Wanaotambaa au kuchukua maumbo ya wanyama (kama nyoka Paka au hata mbwa weusi) na wengine: ni wale wanaoishi maeneo maalum na kutembea kama binadamu.

MAKAZI YAO: Wanapendelea kuishi maeneo yaliyotengwa kama vile mapango, bahari, majalala, nyika, na nyumba zilizoachwa tupu kwa muda mrefu ‘maghofu’.

JINSI JINI ANAVYOWEZA KUMDHURU AU KUINGIA KWENYE MWILI WA BINADAMU:

Wanachuoni wengi wanakubali kuwa jini anaweza kuingia au kuathiri mwili wa binadamu kutokana na sababu kadhaa:

Kisasi: Binadamu anapomdhuru jini bila kujua (mfano: kumwaga maji ya moto pasipo kutaja jina la Mungu).

Mapenzi: Jini wa kiume kumpenda mwanamke wa kibinadamu (au jini mwanamke kumpenda mwanamume), maarufu kama Jini Mahaba.

Kutumiwa kupitia Uchawi: Jini anapotumwa na mchawi kwenda kufanya uharibifu, au kumdhuru mtu aliyelengwa ‘kunuwiwa’ katika uchuwi huo.

Hali za Ghafla: Jini anaweza kuingia mtu anapokuwa na hofu kubwa iliyopitiliza, hasira kali sana, au kughafilika kiimani, Lakini wengine huenda mbali zaidi na kusema haswa kwa WANAWAKE ‘wakiwa wachafu kama wanamilikiwa na viumbe hawa basi watawapanda kwa kuwa hawapendi seemu iliyo chafu. (Dhahiri: Kwenye baadhi ya shule za mabinti pekee, sio nadra kusikia Fulani kapandisha ‘mapepo’)

 


ELIMU KUHUSU UCHAWI

Uchawi ni vitendo vinavyofanywa na binadamu kwa kushirikisha nguvu za giza (Kutumika kwa majini wabaya au mashetani kama nlivyoeleza hapo juu) ili kubadilisha uhalisia wa mambo au kusababisha madhara kwa mtu mwingine.

KIJAMII: Aina za Uchawi Zinazozungumzwa ni zile za, Kurithishwa / Asili, Kununua, na kwa kujifunza, ambapo “Kiasili – Siri za uchawi zinarithiwa ndani ya familia au ukoo tangu utotoni kizazi na kizazi ‘generation to generation’.

·       Uchawi wa Kujifunza: Mtu anapoenda kwa waganga au wachawi wakubwa ili kufundishwa mbinu na miiko ya uchawi.

·       Uchawi wa Kutupiwa (Vifungo na Magonjwa): Kutumia majini au madawa ya kigiza kumfunga mtu kimaisha, kumfanya mgonjwa, au kuharibu ndoa na biashara yake.

Dalili Zinazohusishwa na Uchawi au Kusumbuliwa na Majini:

Kulingana na matatibu wa tiba asilia na za kidini, mtu aliyeathiriwa na uchawi au majini wabaya anaweza kuonyesha dalili mbalimbali kama vile:

·       Maumivu ya mwili yasiyoonekana kwenye vipimo vya hospitali (kama kifua kubana au moyo kwenda mbio).

·       Kuota ndoto za kutisha mara kwa mara (kama kufukuzwa na wanyama wakali, kuanguka kutoka sehemu ndefu, au kufanya tendo la ndoa ndotoni).

·       Kuchukia ghafla mambo ya ibada au kuhisi uzito mkubwa unapotaka kusali au kusoma vitabu vitakatifu.

·       Mabadiliko ya tabia ya ghafla, mfano: mke kumchukia mume au mume kumchukia mke bila sababu ya msingi.

·       Kuhisi ganzi, joto kali, au baridi isiyo ya kawaida kwenye viungo vya mwili.

 


KINGA NA TIBA DHIDI YA UCHAWI NA MAJINI

Katika mifumo yote ya imani, suluhisho kubwa la kujikinga na nguvu hizi hutegemea kumkaribia Mwenyezi Mungu na kufanya ibada ‘Dua’ kwa kumcha yeye pekee, na kwa waKristo (Kufanya Maombi) kwa kuliita na kulitaja jina la YESU inatosha kukuepushia na maswahibu yote hayo.

·       Nguvu ya Jina la Yesu: Wakristo huamini kuwa mapepo (majini wabaya) na nguvu za uchawi hushindwa kupitia maombi ya damu na jina la Yesu Kristo.

·       Kufunga na Kuomba: Kutenga muda wa maombi maalum ya kuvunja vifungo vya kigiza.

·       Kuishi Maisha ya Utakatifu: Kujiepusha na dhambi ili kuzuia shetani kupata mlango wa kuingia kwenye maisha yako.

Mbali na hilo kwa upande mwingine wa UISLAMU tiba imeelezwa ni kufanya (Tiba ya Ruqya), Kusoma Quran: Kutumia aya za Quran na dua zilizofundishwa na Mtume Muhammad (S.A.W), wakitumia Surah maarufu kwa kinga iitwayo (Ayat al-Kursi, Surah Al-Ikhlas, Surah Al-Falaq, na Surah An-Nas)

·       Dua za Asubuhi na Jioni (Adhkar): Kinga kulinda mwili na nyumba dhidi ya mashetani.

Kujiepusha na Ushirikina: Inashauriwa na ni marufuku kwenda kwa waganga wa kienyeji wanaotumia majini kutoa tiba, kwani kufanya hivyo ni kumuasi Mwenyezi Mungu na kuongeza matatizo kwenye maisha ya muhusika atakayefanya shirki ‘Ushirikina’.

Tahadhari ya Kiteknolojia na Kijamii:

Katika ulimwengu wa sasa, kuna kurasa nyingi za mitandao ya kijamii na tovuti zinazodai kufundisha namna ya kuwamiliki au kuwatumia majini kwa ajili ya utajiri, Kununua pete, na vito mbalimbali ili kupata nguvu hizo za kichawi, zaidi sana zinazotumiwa na waganga.

Viongozi wengi wa dini wanaonya vikali dhidi ya kutembelea au kusoma maudhui haya, kwani yanatajwa kuwa ni mitego inayoweza kumuingiza mtu kwenye matatizo makubwa ya kisaikolojia na kiroho, kwa kuamini kile asichokiamini; – Maana imeelezwa kuwa ‘Imani huumba’

EPUKA KUAMINI, NA ISHI KWA KUMTEGEMEA MUNGU PEKEE KATIKA MAJARIBU NA MASWAHIBU UNAYOKUTANA NAYO, MAANA YEYE NDIE MUHUKUMU WA MWISHO, KWENYE MAISHA HAYA NA BAADA YA MAISHA HAYA.

Tufuatilie hapa tafadhali (bofya kiungo chini kwenda facebook Page):

#SirMeena: Waweza kuniandikia maoni yako na tukajadili pamoja....

Je! Kuna uhusiano kati ya Imani hizi na Fremason? Hili nalo ni fumbo jingine! Tuishie hapa kwa Leo. ASANTE!

No comments:

Post a Comment