Mila na desturi za makabila mbalimbali hupaswa kuenziwa na kuendelezwa na jamii husika, (haswa tamaduni nzuri na kutokomeza zile mbaya) ambapo kwa pamoja leo naomba tuangazie kuhusu utamaduni wa Wafipa Urithi wa Mali, Mke baada ya msiba.
UTARATIBU WA KUMALIZA MISIBA NA URITHI
Katika kumaliza kilio kwa Wafipa, jambo la kwanza ambalo mpaka sasa linafanyika ni kuitishwa kwa mkutano wa awali wa ndugu ukiongozwa na Mzee wa boma au wakuu wa ukoo wa kila upande mume na mke, ambapo kwa pamoja hujadili nani atamrithi marehemu (kwa lugha ya kifipa ikijulikana kama ‘akakwiliya’.)
Wanaoweza
kurithiana ni watoto wa baba mkubwa na mdogo, watoto wa mama mkubwa na mdogo, Binamu
na pia mtoto anaweza kumrithi baba yake kama ndugu za huyo baba wameisha (hata
hivyo urithi huo ni wa kusaidia kumtunza mjane au mgane na sio kuchukua uhusika
wa kuwa mke na mume).
Pia
mjukuu anaweza kumrithi babu au bibi kuwa mume wake au mke wake (kama cheo cha
kupewa tu), Mtu na kitukuu wanarithiana kwa hali na mali yaani wanaweza
kuchukuliana mke na mume, mtu anaweza kumrithi mjomba wake na mke wa mjomba
akawa mke wake nk.
Lakini
cha kushangaza zaidi katika mila hii ya kurithiana: Msichana anaweza kumrithi
shangazi yake na mume wa shangazi akawa mume wake, ambapo Zamani ilikuwa hata
shangazi akiwa hai, mathalani akiumwa kwa muda mrefu msichana (Mpwa) wa
shangazi alipelekwa kwa shangazi yake ili kumsaidia katika kazi zote hata
kulala na baba (Mume wa shangazi) ili kumzuia mumewe huyo asilale nje ya ndoa. Pagumu
hapo! Nikulala tu sijui kama kuna mengine yanaendelea……
Zamani
mrithi hukabidhiwa mali zote za marehemu (haswa mume) ikiwa ni pamoja na mke na
watoto wake wote aliokuwa nao na wao kumpa heshima yake kama baba mpya.
Mkutano
huu wa ‘Akakwiiya’ kwanza hufanyika kwa siri kidogo ili wanandugu wawe huru
kujadili nani haswa anastahili kukabidhiwa jukumu hilo la urithi, ambapo baada
ya mkutano huo wa kificho hatimaye hufuatiwa na mkutano wa hadharani ambao kila
mtu anayetaka anaweza kuhudhuria.
Na
mkutano huo unaoongozwa na mkuu wa ukoo kwa upande wa kiumeni, naye huuliza
kama kilio au maombolezo yameisha.! Kama watasema yaendelee, basi anaruhusiwa
kuuendeleza kwa gharama zake, na kama utakuwa umefika mwisho, basi mjadala wa
urithi unafanyika kwa kutoa mapendekezo na maafikiano yaliyopatikana katika
kikao cha uficho.
Kwa
Wafipa wa Milansi kama mtoto wa kwanza katika familia ndiye aliyefariki basi
urithi huenda upande wa baba na anapokufa mtoto mwingine inakuwa zamu ya upande
wa mama wa marehemu.
Baada
ya uamuzi kufikiwa wa nani atakuwa mrithi, basi akina mama walioko kwenye
chumba cha maombolezo hupelekewa taarifa na wakiafiki huitikia kwa kusema ‘Mwandila
ta” na
kama hawakubaliani nao hupewa fursa ya kutoa mawazo yao.
Endapo
akina mama wamekubaliana na uteuzi wa mrithi, basi mama mmoja huchaguliwa
kufagia eneo ambalo mfiwa alikuwa analala, ambapo kama mrithi ametoka upande wa
kiumeni basi mfagiaji huwa wa upande wa kikeni na lazima pafagiliwe siku hiyo
hiyo.
Kwa wafipa vumbi linalotolewa baada ya kufagia eneo ambalo mfiwa
alikuwa analala linamwagwa chooni, Hii ni kwa ajili ya tahadhari ya mchawi
kuchukua vumbi hiyo na kufanyia uchawi kama inavyoaminika.
Kadhalika, mtu haruhusiwi kuchukua mifupa ya nyama ya kilioni na
hii ni kwa tahadhari ya mtu kufanyia uchawi kama Wafipa wanavyoamini.
Baadaye
watu wote hutangaziwa mrithi ni nani na hapo hutolewa chakula na baada ya
chakula watu huondoka.
Kayeemba
hupewa nafasi ya kumnawisha mrithi miguu, mikono na uso kwa maji ya uvuguvugu
na kisha humpaka mafuta; ikiwemo Vifaa vyote ambavyo vimerithishwa navyo pia
hupakwa mafuta.
Baada ya kupewa vifaa vya urithi husindikizwa kutoka nje ya
nyumba na kutembea hatua chache nje ya nyumba na baadaye kurudi. (Hii inakuwa ni
kukumbusha vitendo vya marehemu kuwa alikuwa anatoka na kurudi.)
Tendo
hilo likishafanyika, hutolewa nje viti viwili vinavyokaliwa na mrithi na
mrithiwa na hii inakuwa fursa ya kupewa mawaidha kwa lugha ya Wafipa huita ‘Ukusuunda’
na baada ya mawaidha hayo kutolewa hufuatiwa na
kitendo cha kunyolewa nywele wahusika.
Kwa
Wafipa kuonesha huzuni ya kufiwa, wote hupaswa kunyoa nywele zote
kichwani (kipara)
na hili hufanyika kwa ndugu wote wa marehemu, ambapo Kwa kawaida mrithi na
mrithiwa hupaswa kunyoana wenyewe, kisha baada ya kumaliza msiba ilikuwa ni shurti
kuenda kuoga maji ya mtoni.
Wakati
wa maombolezo, waombolezaji hawakuoga; Hivyo baada ya kunyolewa nywele huenda
kuoga au kunawa, ikiwa ni njia ya kujitakasa na pepo wabaya ambao wanaweza
kuleta kifo.
Pombe ya asili ya kabila la Wafipa inayotengenezwa kwa ulezi na
kunyewa kwa kwa kutumia mirija. |
Baada
ya hapo kinatolewa chakula cha jioni. ‘i chiloosha’. Mkuu wa ukoo wa upande wa baba alikula kuku na
kwa heshima sana alipewa filigisi ‘i’inkushu’ ambayo kwa Wafipa ni
nyama ya heshima sana (hailiwi na wote). Naye humega na kugawa kidogo kidogo
kwa baadhi ya wanaukoo.
Mjumbe
au mkuu wa kijiji naye alichinjiwa kuku, ikiwa ina maana kuku wa kusafisha mji,
na huyo kuku aliliwa na jumbe pamoja na wazee wengine wa kijiji ili kukisafisha
hicho kijiji. Hii kwa wale wapenda kuku, siku kama hizo hawazikosi….
Moto
wa kilioni pia huzimishwa siku hiyo na mzimishaji huwa ni kayeemba, na Majivu yote hutupwa
chooni pia. Kuzimwa kwa moto huo huonesha kwamba kilio kimeisha.
HIYO
NI KUHUSIANA NA UTAMADUNI WA WAFIPA KATIKA KUMALIZA MISIBA, NA UTAMADUNI WA
KURITHISHANA MALI NA WATU – uonavyo wewe ipi hasara na faida ya tamaduni hii….?
SOURCE: January Mbalamwezi (mwandishi wa kitabu cha ‘Utamaduni wa Wafipa)
- Wakuu wa Sumbawanga
- Habari Leo (Makala 18792)
- The white Fathers na Ufipa.
- Channel 10.
TOLEO
LIJALO: TUTAANGAZIA KUHUSU ASILI YA NENO SUMBAWANGA NA MWANZILISHI WAKE!
Share Pia kama umeipenda na wenzako pia waone na kujifunza.
No comments:
Post a Comment