Friday, 20 October 2017

HARUFU MBAYA YA KINYWA ISIKUFANYE UKOSE KUJIAMINI MBELE YA WENZAKO

Namna sahihi na njia bora ya kusafisha meno, hushauriwa kuwa usiku kabla ya kulala na asubuhi kabla ya kupata kifungua kunywa.

Afya ya kinywa ina umuhimu mkubwa zaidi ya unavyoweza kufikiria kwani huweza kumuweka muhusika katika hali ya kujiamini au kutokujiamini mbele ya wenzake.
 
Ambapo mara nyingi, mtu anaposumbuliwa na kutoa harufu mbaya kinywani, huweza kutengwa waziwazi na wenzake wakiwa katika makundi wakiongea kutokana na harufu mbaya itokayo kinywni na ambayo huwa sio rahisi kuvumilika.

TAMBUA TATIZO:

Kwa ujumla tatizo hili hutokana na muhusika kutokujiwekea utaratibu mzuri wa kusafisha kinywa chake kwa muda mrefu, kutumia mswaki mmoja muda mrefu, pamoja na kuswaki pasipo kuchokonoa mabaki ya vyakula yagandayo kwenye fizi za meno kwa kutumia nyuzi zinazoshauriwa na wataalamuau kutumia vijiti vya meno (tooth-stick) baada ya kula.
 
Mara nyingine muhusika kutokuwaona wataalamu ili kupima na kujua namna ipasayo kuweza kutunza meno yake, au kupewa ufahamu kuhusiana na jinsi afya yako ya mwili ilivyo.
 
Kuelezewa uhusiano uliopo kati ya afya ya kinywa na afya ya mwili mzima kunasaidia kufahamu umuhimu wa kutunza kinywa na hasa meno yako na fizi.
 
Kama zilizo sehemu nyingine za mwili, kinywa nacho kimejaa bakteria ambao wengi wao hawana madhara katika mwili wa binadamu, ambapo Kwa kawaida mfumo wa kulinda mwili na utunzaji mzuri wa kinywa kama vile kupiga mswaki na kutumia uzi kuondoa uchafu katika meno kunaweza kudhibiti bakteria walioko kinywani wabakie katika hali ya kawaida na kutodhuru kinywa chako.
 
Lakini bila kutunza vyema kinywa chako, bakteria hao huweza kusababisha maambukizo kutoka jino moja hadi jino jingine na kusababisha meno yako kuoza na hatimaye kupata maradhi ya fizi, au kung’oa meno yote na kubakia kibogoyo (kutokuwa na meno).
 
NAMNA SAHIHI YA UTUNZAJI WA KINYWA CHAKO
Afya ya kinywa inajumuisha siha na namna ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo hasa meno na fizi, pamoja na namna iliyobora ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo wako zinazofikika na zisizofikika hasa meno na fizi.
 
Mbali na kinywa kutuwezesha ipasavyo kula, kuzungumza na hata kuwa na muonekano mzuri wa uso (kutabasamu na kucheka mbele ya wengine), meno na fizi zinapaswa zisiwe zimedhurika na kuwa na matatizo kama vile meno kuoza, magonjwa ya fizi, kung'oka meno na mdomo kunuka.
 
Kuoza meno na meno kuwa na matundu ni matatizo ya kinywa yanayoshuhudiwa sana miongoni mwa watu wengi kwa miaka ya sasa hasa vijana, ambapo katika rika la miaka 20 – 38 tayari muhusika anakuwa ameng’oa meno mpaka matatu.
 
Sababu zinazoweza kuzuia matatizo hayo ya meno ni kudumisha usafi wa kinywa mara kwa mara, kupata fluoride ya kutosha na kutokula kwa wingi vyakula vinavyoweza kudhuru meno na kusababisha matundu hayo.
 
UHUSIANO AFYA YA KINYWA NA MENO
Afya ya meno na kinywa kwa ujumla inahusiana na afya ya mwili mzima kwa njia tofauti, na aina ya vyakula unavyopendelea kula; sababu kuwa na uwezo wa kutafuna chakula na kukimeza ni muhimu ili mwili wako uweze kupata virutubisho muhimu vya kujenga mwili.
 
Halikadhalika kuwa na kinywa chenye matatizo huweza kuathiri namna mtu anavyozungumza na hata kujiamini kwake mbele za watu walio karibu, kupunguza ufanisi kwa wanandoa, pia matatizo hayo ya meno yanaweza kupelekea gharama kubwa ya matibabu na ukarabati wa meno yako.
 
SABABU ZINAZOPELEKEA KUATHIRI AFYA YA KINYWA NA KUTOA HARUFU MBAYA MDOMONI
Mfano wa mpangilio wa meno, na namna ya fizi zinavyoweza kudhuru meno mdomoni, meno kuwa imara au meno kutotoba.


 

Uimara wa meno na fizi hutofautiana sana kati ya mtu na mtu, na umbo la taya zake, muundo wa mdomo na mpangilio wa meno yake, na hata kiasi cha uchache au wingi wa mate mdomoni mwako.
 

Baadhi ya watu ambao hupendelea kula mara kwa mara vyakula venye sukari nyingi na vyenye siagi, imeeleza na wataalamu kuwa watu hao kwa asilimia kubwa ndio wamekuwa wakisumbuliwa zaidi na matatizo haya, kwani huzalisha kemikali nyingi mdomoni ambazo huruhusu wingi wa asidi au tindikali ambayo nayo humpelekea muhusika kujawa na mate mengi mdomoni.
 
Ambapo kujawa mate huko mdomoni hupelekea kukosa kujiamini kwa muhusika mbele ya wenzao, iwe wakati wa kuongea  au kucheka kwani wamekuwa wakirusha chembe-chembe za mate ambazo huwatoka vinywani mwao pasipo wao wenyewe kujitambua au kuweza kujizuia, na ikifikia wakati huo watu hawa ndio hutengwa waziwazi na wenzao.
 
Kwa uchache, Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yanayoweza kuainishwa kwa nini baadhi ya watu meno yao yanaoza zaidi kuliko wengine, kutoa hurufu mbaya kinywani na kukosa kujiamini au pia baadhi ya watu kuwa na meno dhaifu na wengine kuwa na meno yaliyo imara.
 
SABABU ZA KUTOBOKA KWA MENO
Baadhi ya meno yanaweza kutoboka kwa kuwa na vishimo na nyufa ambazo huweza kuruhusu bakteria na tindikali kupenya kwa urahisi, kutokana na kutafuta sehemu salama ya kujihifadhi ili wasishambuliwe na tindikali hiyo.
 
Ambapo kutokana na nyufa zilizoko katikati ya meno huruhusu mabaki mengi ya vyakula kutwama kwa muda mrefu, na kutoa ulinzi kwa baikteria shambulizi wa meno kutoshambuliwa na tindikali-mate, kwani wakati muhusika akiswaki au kusafisha kinywa chake hushindwa kuzisafisha sehemu hizo zenye mabaki ya vyakula.
 
Na hiyo huchagizwa na maumbo ya baadhi ya taya za watu hao, ambapo taya zao na mpangilio wa meno yao huweza kuzuia meno yasisafishike vizuri na kuondoa vyema uchafu kinywani ulioko katikati ya meno yao “hapa fahamu mpangilio wa meno yako na namna sahihi ya usafishaji wake”.
 
Kiwango cha mabaki ya vyakula vingi haswa vyenye sukari, na uchache wa mate yalivyo mdomoni pia huweza kuathiri uozaji wa meno yako na kutobolewa au kushambuliwa kwa urahisi na wadudu wavamizi.
 
Kwa mfano matundu na nyufa za meno huwa haziko sana katika meno ya mbele ambako kuna mate mengi, ikilinganishwa na meno ya nyuma.
 
Ndio maana meno mengi yanayoanza kushambuliwa na wadudu huwa ni meno ya nyuma (magego) kuliko meno yaliyoko upande wa mbele.
 
KUNUKA KWA MDOMO NA NAMNA SAHIHI YA KUZUIA HARUFU MBAYA YA KINYWA
 
Kutoa harufu mbaya kinywani, huchagizwa na kutokupiga mswaki mara kwa mara, kutumia mswaki mmoja muda mrefu, kutojiwekea utaratibu wa kusafisha mabaki ya chakula yaliyotwama katikati ya meno yako au kwenye fizi.
 
Kupiga mswaki au kusafisha kinywa chako, unashauriwa na wataalamu wa meno kufanya hivyo walau mara mbili kwa siku; ikimaanisha usiku kabla ya kulala na asubuhi kabla ya kupata kifungua kinywa.
 
Watu wengi hapa mmekuwa mkikosea namna bora ya kusafisha kinywa chako, kwa kupiga mswaki na kisha kula ‘hiyo ni makosa’.
 
Wataalamu wanakwambia muda ambao wadudu wanaoshambulia meno (baikteria) ni majira ambayo unakuwa mwili umejipumzisha, na mdomo wako haufanyi kazi “kula au kuongea” hivyo wakati gani muhimu zaidi kwako kupiga mswaki? Jibu unalo!
 
Kuzuia harufu mbaya ya kinywa chako; hakikisha unaswaki mara baada ya kula na kabla ya kulala, ikimaanisha ukishamaliza kula pumzika dakika25 au 30, kisha piga mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye fluoride na madini ya ‘calcium’ kwa wingi.
 
Asubuhi ukishapiga mswaki na kupata kifungua kinywa hakikisha unasukutua maji mdomoni mwako kuondoa mabaki ya chakula au vitafunwa kwenye meno yako.
 
Mwisho kabisa, waone wataalamu kuchunguza afya ya kinywa chako mara kwa mara, kupata ushauri wa namna ya kutunza meno yako yasishambuliwe na wadudu, pamoja na kujiwekea utaratibu wa kusafisha fizi zako kwa kutumia uzi angalau mara3 kwa wiki.
 
Stewart Meena:

No comments:

Post a Comment