Fujo zimezuka katika mji mkuu wa Gabon, Libreville baada ya Rais Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi.
Mgombea wa upinzani Jean Ping amesema watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vikosi vya usalama kuvamia makao makuu ya chama chake.
Serikali imesema inawaandama "wahalifu wenye silaha" ambao awali walikuwa wameteketeza majengo ya bunge
Wakati huohuo:
Kwa upande wake mgombea huyo aliyeshindwa amesema pia vikosi vya usalama vimeshambulia makao yake makuu kwenye mji mkuu Libreville.
Jean Ping aliliambia shirika la habari la ufaransa AFP kuwa vikosi vya ulinzi vimetumia helkopta kushambulia kwa mabomu jengo hilo kabla ya kulivamia.
Amearifu kuwa watu 19 wamejeruhiwa baadhi yao wakipata majeraha mabaya.
Awali, polisi katika mji mkuu wa Gabon, Libreville walitumia mabomu ya kutoa machozi kuweza kuwatawanya wafuasi wa Jean Ping, waliokuwa wamejawa na hasira na ambao wanaamini kuwa matokeo hayo ya uchaguzi yalikuwa ya udanganyifu.
Ni kura chache tu, zilizomuwezesha Bwana Bongo kumshinda mpinzani wake na hatimaye kutangazwa kuwa mshindi, huku eneo analotoka akionekana kupata kura nyingi zaidi.
Ujumbe uliokuwa ukiwakilisha upinzani katika Tume ya Uchaguzi ulitoka nje na kukataa kusaini karatasi, zinazompa ushindi Rais Bongo.
Mwangalizi wa Uchaguzi huo, kutoka Jumuia ya Ulaya, Sara Crozier ameelezea hali ilivyo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Libreville, kuwa ni ya wasiwasi.
Familia ya Bongo imekuwa madarakani katika nchi hiyo ya Afrika ya kati kwa takriban miongo mitano.
SOURCE: BBC swahili
No comments:
Post a Comment