Source: BBC SWAHILI http://www.bbc.com/swahili/habari-41084338
Ni kwa nini Korea Kaskazini inataka silaha za nyuklia?
Rasi ya Korea iligawanyika na kuwa mataifa mawili baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kukawa na Korea Kaskazini na Kusini.
Korea Kaskazini iliegemea siasa za Kikomunisti na iliongozwa na serikali ya kiimla, uongozi sawa na wa Stalin katika Muungano wa Usovieti. Marafiki wake wakuu ni Urusi na Uchina.
Nchi hiyo ilijitenga pakubwa na nchi nyingine, isipokuwa nchi kadha marafiki wake.
Viongozi wa nchi hiyo wanasema silaha za nyuklia ndiyo njia pekee ya kujikinga dhidi ya maadui kutoka nje ambao wanataka kuliangamiza taifa hilo.
Majaribio yake ya karibuni zaidi ya makombora yanaachilia kwamba nchi hiyo inakaribia sana kuwa na makombora ya kuruka kutoka bara moja hadi jingine yanayofahamika kama (ICBM) ambayo yana uwezo wa kufika Marekani bara.
Wamefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano. Taarifa za kijasusi zinadokeza kwamba nchi hiyo inakaribia sana, au tayari imeweza, kuunda kichwa kidogo cha silaha za nyuklia kinachoweza kuwekwa kwenye makombora.
Nchi hiyo inaichukulia Marekani kuwa audi wake mkuu na pia ina maroketi ambayo yameelekezwa kwa Korea Kusini na Japan, nchi ambazo zina wanajeshi wengi sana wa Marekani.
Nini kimefanywa kuwazuia?
Juhudi za kutumia mashauriano kutatua mzozo huo zimeshindwa kupata suluhu.
Umoja wa Mataifa umeiwekea nchi hiyo vikwazo vingi - lakini bila mafanikio.
Uchina, mshirika wake wa dhati, pia imeiwekea shinikizo za kiuchumi na kidiplomasia.
Marekani sasa imetishia kutumia nguvu za kijeshi na Rais Donald Trump ameitahadharisha kwamba itakabiliwa kwa "moto na ghadhabu".
President: Kim during Press conference in North Korea |
Marekani inaweza kuishambulia Korea Kaskazini?
Mzozo huo umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi, lakini hali kwamba Korea Kaskazini inakaribia kuwa na/ au tayari ina uwezo wa kuunda kichwa kidogo cha nyuklia kinachoweza kuwekwa kwenye makombora, na kwamba ina makombora yanayoweza kufikia Marekani bara, yanabadilisha mambo sana.
Miezi kadha iliyopita, kumekuwa na hatua za 'uchokozi' mara kadha za Korea Kaskazini pamoja na majibizano kati yake na Marekani ambazo zimezidisha mzozo huo.
Korea Kaskazini ilitishia kurusha mabomu karibu na kisiwa cha Guam ambacho kinamilikiwa na Marekani katika Bahari ya Pacific.
Na leo Jumanne, nchi hiyo imerusha kombora kupitia anga ya Japan.
Lakini huku majibizano yakiendelea, bado ni vigumu kubashiri ni nini kitafuata.